KILIMANJARO WANANCHI WAJITOKEZA KWA WINGI KUPATA ELIMU NA MSAADA WA KISHERIA: MATUKIO KATIKA PICHA

Mnamo tarehe 29 Januari 2025, Wizara ya Katiba na Sheria ilizindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Mkoa wa Kilimanjaro. Uzinduzi huo ulifanyika katika viwanja vya Stendi ya zamani, ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kupata huduma za kisheria. Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, aliongoza uzinduzi huo na kueleza kuwa kampeni hii inalenga kutatua migogoro mbalimbali inayowakabili wananchi. Alisisitiza kuwa kampeni hii ni utekelezaji wa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa urahisi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliwahimiza wananchi kutumia fursa hii kupata elimu na msaada wa kisheria ili kutatua changamoto zinazowakabili.