Kongamano la Msaada wa Kisheria la Mwaka 2025 limezinduliwa rasmi jijini Arusha katika hafla iliyoambatana na ujumbe mzito kuhusu haki, usawa na wajibu wa pamoja katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata msaada wa kisheria bila vizingiti. Uzinduzi huo umeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu Eliakim Chacha Maswi, ambaye amesisitiza dhamira ya serikali ya kuendeleza haki jumuishi kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya sekta ya sheria. “Msaada wa kisheria si jambo la hiari tena – ni msingi wa utawala wa sheria na haki za binadamu. Ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha kuwa haki haibagui, haicheleweshwi na haikimbiwi na mwananchi kwa sababu ya umasikini au kutokujua,” alisema Maswi katika hotuba yake ya uzinduzi. Kongamano hilo limewaleta pamoja viongozi kutoka taasisi za kisheria, wanasheria wa kujitolea, wanataaluma, asasi za kiraia, na wawakilishi wa mashirika ya maendeleo. Washiriki wamejadili kwa kina changamoto, mafanikio na mikakati mipya ya kuimarisha...