UZINDUZI WA KONGAMANO LA MSAADA WA KISHERIA 2025 LAFANA JIJINI ARUSHA
Kongamano la Msaada wa Kisheria la Mwaka 2025 limezinduliwa rasmi jijini Arusha katika hafla iliyoambatana na ujumbe mzito kuhusu haki, usawa na wajibu wa pamoja katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata msaada wa kisheria bila vizingiti.
Uzinduzi huo umeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu Eliakim Chacha Maswi, ambaye amesisitiza dhamira ya serikali ya kuendeleza haki jumuishi kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya sekta ya sheria.
“Msaada wa kisheria si jambo la hiari tena – ni msingi wa utawala wa sheria na haki za binadamu. Ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha kuwa haki haibagui, haicheleweshwi na haikimbiwi na mwananchi kwa sababu ya umasikini au kutokujua,” alisema Maswi katika hotuba yake ya uzinduzi.
Kongamano hilo limewaleta pamoja viongozi kutoka taasisi za kisheria, wanasheria wa kujitolea, wanataaluma, asasi za kiraia, na wawakilishi wa mashirika ya maendeleo. Washiriki wamejadili kwa kina changamoto, mafanikio na mikakati mipya ya kuimarisha msaada wa kisheria nchini.
Wakili Boniface Mwabukusi, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambaye amehimiza mshikamano wa kitaifa katika kutoa msaada wa kisheria hasa kwa makundi maalum kama wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
Bi Ester Msambazi, Mkurugenzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria, ambaye ameeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia kampeni hiyo ikiwemo uanzishaji wa vituo vya msaada wa kisheria kwenye wilaya mbalimbali, na elimu kwa jamii kuhusu haki zao.
Kongamano hili la siku kadhaa linatarajiwa kuibua mapendekezo yatakayoimarisha sera, mifumo na ushirikiano katika utoaji wa msaada wa kisheria nchini. Pia, litakuwa fursa ya kuwakutanisha wadau kwa mafunzo, mijadala ya kitaalamu na maonyesho ya huduma zinazohusiana na haki.
Kwa mujibu wa Wizara ya Katiba na Sheria, maazimio yatakayopitishwa yatasaidia kuboresha mikakati ya kitaifa ya kuhakikisha kuwa huduma ya msaada wa kisheria inawafikia wananchi wote, hususan maeneo ya vijijini na mijini yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma hizo.
Comments
Post a Comment