MSLAC - KUONGEZA HAKI NA UELEWA WA KISHERIA KWA JAMII

 Kampeni hii ya miaka mitatu, kuanzia Machi 2023 hadi Februari 2026, inalenga kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi, hususan katika masuala muhimu kama ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yanayohusiana na haki za binadamu kwa ujumla. 


Utekelezaji wa kampeni hii unafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara na Taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia, Wanazuoni, na Wadau wa Maendeleo. Lengo kuu la kampeni hii ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini Tanzania. 


 

Kwa kufikia lengo hili, kampeni inalenga kuongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu, kutoa huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia, na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu elimu ya sheria, masuala ya haki na wajibu, na misingi ya utawala bora. 

 


Matokeo ya muda mrefu ya kampeni hii ni kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususan wanawake, watoto, na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi. Kampeni pia inalenga kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja, na kuleta utengamano wa kisiasa nchini Tanzania.

 


 Matokeo ya kati ni kuimarika kwa mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa. Matokeo ya muda mfupi yanajumuisha kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotoa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kupungua kwa idadi ya migogoro na matukio yanayotokana na ukosefu wa uelewa wa sheria, na kuimarika kwa uwajibikaji na uwezo wa taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali zinazotoa huduma za msaada wa kisheria.


 

 Kampeni hii ilianza kutekelezwa Jijini Dodoma tarehe 28 Mei 2023, baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), tarehe 27 Mei 2023. Ratiba ya utekelezaji wa kampeni hii kwa mwaka 2023 imezingatia usawa wa kikanda kwa lengo la kuhakikisha huduma hii inafikia kila kona ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kampeni hii ina msaada mkubwa kwa jamii ya sasa, hususan wale walio mbali na huduma za kisheria, kwa kutoa elimu, ushauri wa kisheria, na kusaidia kuboresha mfumo wa utoaji wa huduma za kisheria nchini.



#MSLAC

Comments

Popular posts from this blog