MAKAMU WA RAIS AFUNGUA WARSHA YA UTEKELEZAJI WA MAPENDEKEZO YA TUME YA HAKI JINAI
Warsha ya Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, na Naibu Makatibu Wakuu kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ilifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango. Warsha hiyo ilifanyika Ukumbi wa Kambarage mkoani Dodoma.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Makamu wa Rais alieleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo ni kuhakikisha kuwepo kwa mfumo imara unaizingatia haki na misingi ya utawala bora katika huduma kwa wananchi.
Aliongeza kuwa nia ya dhati ya Rais ni kuleta mapinduzi ya kifikra na mabadiliko ya kimfumo katika utendaji wa taasisi za Haki Jinai nchini. Makamu wa Rais aliwataka viongozi hao kutekeleza kikamilifu mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, akisisitiza kuwa wananchi wameonyesha hitaji la mabadiliko katika utendaji wa taasisi za haki jinai ili kuhakikisha haki inatendeka.
Aliwasihi kufahamu kwa kina mapendekezo hayo na kujipanga vyema katika utekelezaji wake. Aidha, aliwataka viongozi hao kuendelea kuwasimamia na kuwakumbusha watumishi katika Wizara na Taasisi wanazosimamia kuzingatia maadili, weledi, na nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Makamu wa Rais pia alitilia mkazo juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala. Hivyo, aliiagiza TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Katiba na Sheria, pamoja na Wizara ya Ujenzi kushirikiana kikamilifu katika kusimamia uanzishwaji wa ofisi za vyombo vya utoaji haki katika maeneo hayo.
Alisisitiza kuwa utawala bora katika utumishi wa umma ni dhana inayohusisha usimamizi na utekelezaji wa shughuli za kila siku kwa kuzingatia misingi ya sheria, haki, usawa, uwazi, na uwajibikaji.
#MSLAC
Comments
Post a Comment