Rais Samia Kinara Namba Moja wa Kuimarisha Mifumo ya Upatikanaji wa Haki Nchini - Balozi Dkt. Pindi Chana
Balozi Dkt. Pindi Chana amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa haki nchini. Akizungumza katika hafla maalum, Dkt. Chana alielezea jinsi Rais Samia ameonyesha uongozi bora katika masuala ya utawala wa sheria.
"Napenda kumpongeza sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa haki nchini," alisema Dkt. Chana. "Mtakumbuka Mhe. Rais Samia aliunda tume ya haki jinai, tume ambayo ilizunguka Tanzania nzima kukusanya maoni ya jinsi ya kuboresha masuala ya utawala wa sheria."
Dkt. Chana aliongeza kuwa msaada wa kisheria unaotolewa na Rais Samia ni wa kipekee na muhimu sana kwa Watanzania. "Mhe. Rais mwenyewe Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye mtoa msaada nambari moja katika nchi yetu. Makofi mengi sana kwa Rais wetu kwa juhudi zake za kisheria," alisema huku akimpongeza Rais Samia.
Dkt. Chana alielezea jinsi Rais Samia anavyoshirikiana moja kwa moja na wananchi kupitia ziara zake. "Sisi sote ni mashuhuda wa jinsi Rais Samia anavyosikiliza wananchi. Anasimama juu ya gari kuwasikiliza, anafanya mikutano na Watanzania, anasikiliza hoja zao, maombi yao, na kero zao," alisema.
Alisisitiza kuwa juhudi hizi ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025, ambayo inalenga kuboresha utawala wa sheria. "Mhe. Rais Samia yeye mwenyewe siku zote amekuwa mfano bora na ametuelekeza tuende kwa Watanzania, tuwasikilize changamoto zao, hoja zao, na kuwaelekeza jinsi ya kutatua masuala yote ya kisheria," aliongeza Dkt. Chana.
Dkt. Chana alihitimisha kwa kusema, "Kwa kweli sisi Watanzania kwa pamoja tunapaswa kuendelea kumshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Yeye si kiongozi wa maneno tu bali anaonesha mfano dhahiri."
#MSLAC
Comments
Post a Comment