MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AZINDUA KLINIKI YA USHAURI NA ELIMU YA SHERIA KWA UMMA
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, amezindua Kliniki ya Ushauri na Elimu ya Sheria kwa Umma, inayolenga kusogeza huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi. Lengo kuu ni kupunguza migogoro dhidi ya Serikali na kupata suluhu ya changamoto zinazowakabili wananchi.
Kliniki hiyo, iliyoandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Mawakili wa Serikali, ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alitaka viongozi kuweka utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuwaongoza katika taratibu za kupata haki.
Akizindua Kliniki hiyo jijini Dodoma, Dkt. Feleshi alisema kuwa hatua hiyo itaimarisha utawala wa sheria nchini, na pia itachochea mazingira ya amani kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
"Natoa rai kwa Mawakili wote wa Serikali hapa nchini kutenga muda na kusikiliza wananchi kupitia maeneo yao. Pia nawakumbusha wakuu wa mikoa na wilaya ambao bado hawajakamilisha kuteua wajumbe wawili wa kamati za ushauri, wafanye hivyo haraka ili kamati hizo zianze kusikiliza malalamiko ya wananchi kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa," alisema Dkt. Feleshi.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwakumbusha vyama vya Mawakili wa Serikali (TPBA) na Mawakili wa Tanganyika (TLS) kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na kamati za ushauri wa kisheria ngazi za mikoa na wilaya ili kusikiliza malalamiko na kuyatatua kwa wakati.
Kliniki hizi zitaendeshwa na kamati hizo kwa nchi nzima na hivyo wananchi wa Dodoma na mikoa jirani wanakaribishwa kupata huduma ya ushauri wa kisheria bure kuanzia Juni 26 hadi Julai 3, 2024, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo, alieleza kuwa wananchi wakiendelea kutatuliwa kero zao, uzalishaji utaongezeka kwa kasi.
"Serikali kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia imewawezesha wananchi kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kuelewa namna ya kutafuta suluhu ya malalamiko yao. Kero za wananchi ni wajibu wetu, tuendelee kuwa pamoja katika kuzitatua kupitia ushirikiano wetu. Kupitia siku hizi zilizopangwa, wananchi wataelimishwa zaidi ili wapate haki yao na kuwa na amani," alisema Bi. Makondo.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya msaada wa kisheria kupitia teknolojia ya kidigitali na simu za kawaida ili kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.
Comments
Post a Comment