Je!Kila Mtanzania Anayo Haki Ya Kupata Msaada wa Kisheria? 

Serikali ya Tanzania imeendelea kusimamia kwa nguvu utekelezaji wa haki za msingi kwa raia wake kwa kuanzisha na kuendesha kampeni ya msaada wa kisheria bure. Dhamira hii ya serikali inajikita moja kwa moja katika kuhakikisha kuwa haki za msingi zilizowekwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinawafikia Watanzania wote kwa usawa, bila kujali hali zao za kiuchumi au kijamii.

Kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya Katiba ya Tanzania, haki ya usawa mbele ya sheria ni ya kila mtu, na serikali inawajibika kuhakikisha hakuna ubaguzi unaofanyika katika upatikanaji wa haki. Ibara hii inatoa haki kwa kila raia kusikilizwa mahakamani na kupata ulinzi wa sheria kwa usawa, ikiwa ni pamoja na kupinga aina zote za ubaguzi. Kwa maneno ya Katiba, haki si kitu kinachopaswa kupatikana kwa kundi maalum la watu, bali kwa kila raia bila kujali uwezo wake wa kifedha, kijamii, au kijinsia.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria, iliyoanzishwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha haki hizi za kikatiba zinatimia. Msaada huu unalenga kuondoa vikwazo vya kifedha vinavyowakumba Watanzania wengi, hasa wale walio pembezoni mwa jamii kama wanawake, watoto, na watu wenye ulemavu. Kupitia kampeni hii, serikali inatoa usaidizi wa kisheria katika masuala ya ardhi, ndoa, urithi, na masuala mengine ya kijamii yanayowagusa wananchi wa kawaida.

Kampeni ya msaada wa kisheria Ya Mama Samia, ni sehemu muhimu ya dhamira ya serikali kuhakikisha kwamba haki inawafikia Watanzania wote kwa usawa, kama inavyoainishwa na Katiba ya Tanzania. Hii ni hatua muhimu kuelekea kujenga jamii yenye haki na usawa kwa raia wake wote.

Comments

Popular posts from this blog