MTAA WA KAMBARAGE, KATA YA BUTIMBA – MWANZA: SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN (MSLAC) YATUA NA KUHUDUMIA JAMII

Mwanza, Nyamagana – Mpango wa Samia Legal Aid Campaign (MSLAC) umefika rasmi katika Mtaa wa Kambarage, Kata ya Butimba, ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza, kwa lengo la kuwapatia wananchi elimu ya msaada wa kisheria na huduma muhimu za haki za kisheria.  

 

Katika zoezi hili, wananchi wa Kambarage wamepata fursa ya kupata ushauri wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali yanayowagusa, ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa, kesi za jinai, ajira, pamoja na masuala ya ukatili wa kijinsia. Wanasheria na wataalam wa sheria walioambatana na kampeni hii wamekuwa wakitoa elimu ya kuhamasisha wananchi kufuata taratibu sahihi za kisheria katika kutatua changamoto zao.   

Wananchi waliojitokeza wameonyesha kufurahishwa na hatua hii ya MSLAC, wakisisitiza kuwa elimu wanayoipata itawasaidia kuepuka migogoro inayotokana na kutokuelewa sheria. Aidha, kampeni hii inawahimiza wananchi kuandika wosia, kufuata njia mbadala za utatuzi wa migogoro kama usuluhishi na upatanishi, pamoja na kuhimiza jamii kushiriki kikamilifu katika upatikanaji wa haki kwa wote.  

MSLAC itaendelea kutoa huduma za msaada wa kisheria katika maeneo mbalimbali nchini, ikilenga kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa ajili ya kuimarisha utawala wa sheria na upatikanaji wa haki kwa kila Mtanzania.

Comments

Popular posts from this blog