WANANCHI WA KATA YA MISIMA, KIJIJI CHA MSOMERA WILAYA YA HANDENI WAPATA ELIMU YA MSAADA WA KISHERIA KUTOKA MSLAC.
Katika juhudi za kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wananchi, Mamlaka ya Samia Legal Aid Campaign (MSLAC) imefanya mafunzo muhimu kwa wananchi wa Kata ya Misima, Kijiji cha Msomera, kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. Mafunzo haya, ambayo yalilenga kutoa ufahamu kuhusu haki za kiraia, sheria za ardhi, ndoa, mirathi, na utatuzi wa migogoro, yamejizatiti kutoa uwelewa wa kisheria kwa jamii.
Katika mafunzo hayo, wananchi walijengewa uwezo wa kutatua migogoro yao kwa njia ya amani kupitia mbinu za usuluhishi, kujua haki zao katika masuala ya ardhi na familia, na namna ya kulinda mali zao. Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwapa wananchi uwezo wa kuchukua hatua sahihi wakati wanapokutana na changamoto za kisheria.
"Elimu ya msaada wa kisheria ni muhimu sana kwa wananchi wa maeneo ya kijijini. Leo tumeweza kujua haki zetu na jinsi ya kutatua matatizo yetu kwa njia za kisheria. Hii itatusaidia sana katika maisha yetu ya kila siku," alisema mmoja wa wananchi walioshiriki mafunzo hayo.
Hali hii inadhihirisha juhudi za serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wananchi wote, ili kuhakikisha kuwa haki zinapatikana kwa usawa na kwamba wananchi wanapata suluhisho bora kwa migogoro yao.
Mafunzo haya pia ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama tawala ya kuboresha maisha ya wananchi na kuwawezesha kuwa na uelewa mzuri wa sheria zinazowahusu. Wananchi wa Kata ya Misima, Kijiji cha Msomera wameonyesha shukrani kwa kupata fursa hii muhimu, wakisema kuwa inawasaidia kupata suluhisho bora la changamoto zao za kisheria kwa njia za haki na amani.
Comments
Post a Comment