DAWATI LA MSAADA WA SHERIA LAREKEBISHA MIPAKA KATIKA ENEO LA UCHIMBAJI MAWE MLANGARINI

Mlangarini, Arusha – Katika jitihada za kuondoa sintofahamu kuhusu mipaka ya eneo la uchimbaji mawe, Dawati la Msaada wa Sheria kwa kushirikiana na maafisa ardhi pamoja na afisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wamefika katika Kata ya Mlangarini kutoa elimu ya sheria na kusimamia upimaji upya wa eneo hilo. 

Hatua hii imechukuliwa kufuatia mgogoro wa mipaka kati ya wanakijiji wa Mlangarini na Rikitesh Patel, mmiliki wa kiwanda cha kuchakata mawe kwa ajili ya kokoto. Patel alinunua eneo hilo kutoka kwa baadhi ya wenyeji wa kijiji, lakini kulizuka sintofahamu kuhusu mipaka halisi ya ardhi hiyo.  


Wakati wa zoezi hilo, wataalamu wa ardhi walihakiki na kurejelea vipimo upya ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote na kuondoa migogoro isiyo ya lazima. Wananchi walipata fursa ya kuuliza maswali na kupewa ufafanuzi wa kisheria kuhusu umiliki wa ardhi na taratibu sahihi za mauziano ya ardhi ili kuepuka changamoto za baadaye.

Hatua hii imepokelewa vyema na wanakijiji wa Mlangarini, wakieleza kuwa ni hatua muhimu katika kudumisha amani na kuhakikisha kila mmoja anafahamu mipaka yake kihalali. Dawati la Msaada wa Sheria limeahidi kuendelea kutoa elimu zaidi kuhusu haki za ardhi ili kuwaepusha wananchi na migogoro inayotokana na ukosefu wa uelewa wa sheria za ardhi.



Comments

Popular posts from this blog