WAZIRI NDUMBARO AONGOZA KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID ARUSHA, WANANCHI WANUFAIKA NA MSAADA WA KISHERIA

Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, ameendelea kutoa huduma za msaada wa kisheria mkoani Arusha kupitia Kampeni ya Mama Samia Legal Aid. Huduma hizi zinatolewa katika viwanja vya TBA, zikiambatana na maadhimisho ya Wiki ya Wanawake Duniani yatakayofanyika Machi 8, 2025.

 

Katika kampeni hii, wananchi wamejitokeza kwa wingi kupata msaada wa kisheria. Miongoni mwao ni John Kaaya, mkazi wa Arusha, aliyefika Machi 2, 2025, katika mabanda ya Wizara ya Katiba na Sheria yaliyopo viwanja vya TBA, Arusha, ambapo alipatiwa msaada wa kisheria. 

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Jumanne Sagini, amewataka wananchi kutoa maelezo sahihi kwa watoa huduma za msaada wa kisheria ili kufanikisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili, hususan migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa na masuala mengine ya kisheria. Aliyasema haya alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria mkoani Arusha kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. 

 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Paul Makonda, ameagiza watoa huduma za msaada wa kisheria kuhakikisha wananchi wote wanaofika kupata huduma wanasikilizwa na kutatuliwa changamoto zao kikamilifu. Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata haki zao za msingi kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid inayotolewa viwanja vya TBA. 


Wananchi waliofika kupata huduma wameishukuru serikali kwa kuwasogezea huduma karibu, wakisema kuwa imewapa fursa ya kujifunza na kutatuliwa changamoto zao za muda mrefu bila gharama. Wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hii inayolenga kutatua changamoto mbalimbali za kisheria.

Huduma za msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid zinaendelea kutolewa mkoani Arusha, zikiwapa wananchi fursa ya kupata haki zao na ufumbuzi wa changamoto za kisheria zinazowakabili.

Comments

Popular posts from this blog