Wananchi Wamiminika Morogoro Kupata Huduma za Msaada wa Kisheria Bila Malipo
Mamia ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro wamejitokeza kwa wingi katika Kliniki Maalumu ya Msaada wa Kisheria inayofanyika katika viwanja vya Standi ya Zamani, Manispaa ya Morogoro. Kliniki hiyo imeandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Dawati la Msaada wa Kisheria kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Usaili (RITA) pamoja na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).
Huduma zinazotolewa katika kliniki hiyo ni pamoja na ushauri wa kisheria, elimu ya haki za binadamu, masuala ya mirathi, ndoa na talaka, usajili wa vizazi na vifo, masuala ya ukatili wa kijinsia, pamoja na migogoro ya ardhi na ajira. Kliniki hiyo inafanyika kwa muda wa siku mbili mfululizo, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi hususan wale wasiokuwa na uwezo wa kugharamia huduma za kisheria.
Kwa manufaa ya umma wa Tanzania, kliniki kama hizi zinachangia kuimarisha utawala wa sheria, kupunguza migogoro isiyo ya lazima, na kujenga jamii yenye uelewa wa haki, usawa na amani. Serikali imeendelea kusisitiza ushirikiano wa taasisi mbalimbali ili kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia wananchi wote, hususan makundi maalum na yaliyo pembezoni.








Comments
Post a Comment